SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI YAZINDUA VIFAA VYA KILIMO KATIKA JUHUDI ZA KUPIGA JEKI SHUGHULI ZA WAKULIMA.

Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin amesema kwamba serikali yake itaendelea kuweka kipau mbele maswala ya kilimo kwa kuwekeza zaidi katika wakulima wa kaunti hiyo ili kuhakikisha kuna chakula cha kutosha.

Akizungumza katika jumba la kilimo mjini Kapenguria wakati wa kuzindua vifaa mbali mbali kwa wakulima vinavyonuiwa kupiga jeki shughuli zao za kilimo, gavana Kachapin aidha aliwataka wakulima kukumbatia teknolojia katika shughuli zao za kilimo ili kuhakikisha juhudi za kuwekeza katika sekta hiyo zinazoendelezwa na serikali yake haziambulii patupu.

“Hatua hii inadhihirisha kujitolea kwa serikali yangu kuwekeza zaidi katika sekta ya kilimo ili kuhakikisha kwamba kaunti hii inakuwa na chakula cha kutosha. Nawaomba wakulima kukumbatia teknolojia ya kisasa katika kilimo ili kuhakikisha kwamba juhudi zetu kuimarisha kilimo haziambulii patupu.” Alisema Kachapin.

Naibu gavana Robert Komole alisema kwamba hatua ya kuzindua vifaa hivi ni njia moja ya kuendelea kuonyesha uwazi wa utumizi wa fedha katika serikali ya gavana Kachapin ili kuboresha maisha ya wakazi wa kaunti hiyo ya Pokot magharibi.

“Kuzinduliwa kwa vifaa hivi kunadhihirisha wazi uwazi uliopo kwa serikali ya gavana Kachapin. Ingekuwa ni serikali ya kuficha maneno, labda wakulima hawangefahamu ni nini serikali ya kaunti imefanya. Lakini kwa sababu gavana anazingatia uwazi, ameamua kuja mbele ya wananchi kuweka wazi jinsi anavyotumia fedha za umma.” Alisema Komole.

Kwa upande wake waziri wa kilimo na mifugo kaunti hiyo Wilfred Longronyang aliwahimiza wakulima kuhakikisha kwamba wanatunza vyema vifaa ambavyo wamekabidhiwa na kuvitumia inavyostahili ili kuafikia malengo ambayo yanakusudiwa.

“Nawaomba wakulima ambao wamepata vifaa hivi kuvitunza vyema na kuvitumia ili malengo yaliyokusudiwa yaafikiwe. Lengo letu ni kuhakikisha kwamba shughuli za wakulima wetu zinaimarika na kukabili njaa kaunti hii.” Alisema Longronyang.