SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI YAWAHAKIKISHIA WAZAZI MIPANGO YA KUTOA FEDHA ZA BASARI.
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin amewahakikishia wazazi katika kaunti hiyo kwamba serikali yake inaendeleza mikakati ya kuhakikisha wanafunzi wanapata fedha za basari kufanikisha masomo yao.
Akizungumza baada ya kuandaa kikao na wanahabari Kachapin alisema kwamba atahakikisha kila mwanafunzi katika kaunti ya Pokot magharibi anapokea alfu 25 za basari jinsi alivyoahidi kabla ya kukamilika mwaka huu.
Kachapin alisema kwamba nia yake ni kuhakikisha wanafunzi wote katika kaunti hiyo wanapata elimu bila ya changamoto za karo.
“Tuko tayari kusambaza basari jinsi nilivyoahidi na kabla ya mwaka huu kukamilika tutakuwa tumempa kila mtoto shilingi alfu 25. Tumeweka mikakati na nitahakikisha kwamba kila mmoja ambaye amewasilisha makaratasi yake atapokea fedha hizo na hamna hata mmoja atakayefungiwa nje.” Alisema Kachapin.
Wakati uo huo Kachapin alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa tume ya huduma za walimu TSC kaunti hiyo kuhakikisha kwamba wakazi wanapewa kipau mbele katika shughuli ya usajili wa walimu ambayo inaendelea.
“Walimu wengi wamekaa nyumbani zaidi ya miaka 10 na haitakuwa bora iwapo hawa watakosa nafasi. Hii ni haki ya wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi hasa ikizingatiwa ni kati ya kaunti ambazo zina upungufu mkubwa wa walimu. Hivyo tungetaka wakazi wapewe kipau mbele katika usajili huo.” Alisema.