SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI YATIA SAINI MKATABA WA USHIRIKIANO NA MAMLAKA YA KVDA.

Gavana Simon Kachapin na Mkurugenzi wa mamlaka ya KVDA Sammy Naporos.


Na Emmanuel Oyasi.
Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi imetia saini mkataba wa maelewano na mamlaka ya maendeleo ya Kerio valley KVDA ambao utaiwezesha mamlaka hiyo kushirikiana na serikali ya kaunti katika kuendeleza miradi mbali mbali ya maendeleo.
Akizungumza afisini mwake baada kutia saini mkataba huo, gavana Simon Kachapin alisema kwamba hatua hii inalenga kupanua sehemu za ushirikiano baina ya serikali yake na mamlaka hiyo ambayo imekuwa ikitekeleza miradi mbali mbali hasa ya kilimo katika kaunti hiyo.
Gavana Kachapin alisema kwamba ushirikiano huo utahakikisha usalama wa chakula na raslimali ambazo zitawasaidia wakazi wa kaunti hiyo na kutatua tatizo la utovu wa usalama ambalo limekuwepo kwa muda hasa maeneo ya mipakani pa kaunti, chanzo kikuu kikiwa kung’ang’ania raslimali.
“Tumesaini mkataba na mamlaka ya KVDA kupanua sehemu za ushirikiano lengo kuu likiwa kuimarisha huduma kwa wakazi wa kaunti hii, ikiwa ni njia moja ya kuhakikisha kwamba kuna raslimali za kutosha ili kukabili utovu wa usalama ambao mara nyingi huchangiwa na wakazi kung’ang’ania raslimali.” Alisema Kachapin.
Mkurugenzi wa mamlaka hiyo Sammy Naporos alitaja ushirikiano huo kuwa wenye umuhimu mkubwa kwani utapelekea kuimarika uchumi wa wakazi wa kaunti hiyo, kupitia miradi mbali mbali ambayo mamlaka hiyo itakuwa ikifadhili, ikiwemo kuwapa wakulima mafunzo ya jinsi ya kuendeleza shughuli tofauti za kilimo.
“Ushirikiano huu ni muhimu sana kwa sababu utasaidia kuimarisha uchumi wa wakazi wa kaunti hii. ushirikiano huu pia utasaidia kutoa mafunzo kwa wakulima wa kaunti hii ili kuimarisha shughuli zao za kilimo.” Alisema Naporos.