SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI YATARAJIWA KUZINDUA BASARI KWA WANAFUNZI IJUMAA WIKI HII.


Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi inatarajiwa kutoa hundi za fedha za basari kwa wanafunzi wote waliotuma maombi ya kutaka ufadhili huo kuanzia ijumaa wiki hii katika shughuli itakayofanyika shule ya upili ya Ortum.
Kamati ya elimu katika bunge la kaunti hiyo ikiongozwa na mwenyekiti wake ambaye pia ni mwakilishi wadi ya siyoi Esther Serem ilisema kwamba jumla ya wanafunzi alfu 40 walituma maombi yakijumuisha wanafunzi wa shule za upili, vyuo vikuu na hata vya kadri.
“Tunapeana hundi siku ya ijumaa za waliotuma maombi ya kupokea basari. Tulipata jumla ya maombi alfu 40 kutoka kwa wanafunzi wa shule za upili, vyuo vikuu na vile vya kadri na sasa tutahakikisha kila mtu aliyetuma maombi anapata fedha hizo.” Alisema Serem.
Serem alitoa wito kwa wazazi wa wanafunzi ambao watapata fedha hizo za basari kuwahimiza wanao kutia bidii masomoni ikizingatiwa kwamba fedha hizo si za umma bali zimetokana na ushuru ambao unatozwa wananchi.
“Nawahimiza wazazi wa wanafunzi ambao watapata basari hizo kuwahimiza watoto wao kufanya bidii kwa sababu pesa hizi zinatolewa kwa ushuru unaolipwa na wakenya wala si za serikali jinsi ambavyo labda wengi wanadhani.” Alisema Serem.
Wakati uo huo kamati hiyo ilipinga madai kwamba fedha hizo zimetolewa kwa kuwapendelea baadhi ya wanafunzi ikiwataka wakazi kuyapuuza madai hayo wanayosema ni ya kisiasa wakisema kwamba wanafunzi wote waliotuma maombi watapewa fedha hizo.
“Kuna madai ambayo yanaenezwa kwamba fedha za basari zinatolewa kwa mapendeleo ambapo wapo wanafunzi ambao wamepewa huku wengine wakinyimwa. Nawaarifu wazazi kwamba huo ni uongo na ni madai yanayoenezwa kisiasa. Kila mwanafunzi aliyetuma maombi atapata fedha hizo.” Walisema.