SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI YATAKIWA KUIMARISHA MAZINGIRA YA WAFANYIKAZI KATIKA HOSPITALI YA KACHELIBA.

Wafanyikazi wa idara mbali mbali katika hospitali ya kacheliba kaunti ya Pokot magharibi wameitaka serikali ya kaunti kuangazia hali katika hospitali hiyo ili kuwapa mazingira bora ya kufanyia shughuli zao.

Wakizungumza katika kikao na afisa mkuu wa idara ya afya kaunti hiyo, wafanyikazi hao walitaka miongoni mwa maswala mengine, kuongezewa wafanyikazi wengine ili kurahisisha kazi yao, kuimarishwa hali ya vifaa vinavyotumika hospitalini humo pamoja na kuangaziwa mishahara yao.

“Tunaomba serikali ya kaunti kuangazia maslahi yetu katika hospitali hii ya Kacheliba ikiwemo swala la wafanyikazi ambapo tuna wafanyikazi wachache ikilinganishwa na kazi ambazo tunafanya. Pia vifaa hapa ni vichache sana. Tunaomba pia mishahara yetu iangaziwe.” Walisema.

Ni kauli ambazo zilikaririwa na msimamizi wa hospitali hiyo Dkt. Martine Chege ambaye alisisitiza kwamba maswala yaliyoibuliwa na wafanyikazi hao yanafaa kuchukuliwa kwa uzito hasa ikizingatiwa hospitali hiyo inalenga kuhudumu kwa masaa 24.

“Tunaelekea katika mfumo wa kufanya kazi masaa 24. Na kutokana na hili kuna hitaji kubwa la kuongezwa idadi ya wafanyikazi pamoja na kuimarishwa vifaa kwenye hospitali hii.” Alisema Chege.

Kwa upande wake afisa mkuu katika wizara ya afya kaunti hiyo Nelly Soprin alitoa hakikisho la serikali ya kaunti kushughulikia maswala ambayo yameibuliwa na wafanyikazi hao, huku pia akidokeza kwamba serikali ina mipango ya kuwapandisha vyeo wahudumu wa afya baada ya subira ya muda mrefu.

“Tumeyasikia malalamishi yenu na nawaahidi kwamba serikali ya kaunti ipo tayari kushirikiana nanyi kuhakikisha kwamba mnatoa huduma bora kwa wananchi. Kuna swala la kupandishwa vyeo ambapo tunafahamu kwamba wengi wa wahudumu hawajapandishwa kwa muda. Hilo pia tunaliangazia.” Alisema Soprin.