SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI YASUTWA KWA ‘UTENDAKAZI DUNI’.


Seneta wa kaunti hii ya Pokot magharibi Samwel Poghisio amewasuta vikali viongozi wa kisiasa katika kaunti hii ambao wanawania nyadhifa za uongozi katika uchaguzi mkuu wa mwezi agosti, anaodai kuwa wanatafuta uungwaji mkono wa wananchi kwa kumharibia sifa machoni pa wakazi hali wamechangia kudorora kaunti hii kimaendeleo.
Akizungumza na kituo hiki seneta Poghisio amesema kuwa sekta muhimu katika kaunti hii zimeathirika pakubwa chini ya utawala wa gavana wa sasa John Lonyangapuo na mwaniaji kiti cha useneta Geofrey Lipale ambaye pia amehudumu katika wizara ya afya na kisha ile ya kilimo na mifugo chini ya serikali ya gavana lonyangapuo.
Poghisio ameendelea kuibua maswali kuhusiana na matumizi ya fedha ambazo serikali ya kaunti hii imepokea kutoka kwa serikali kuu hali hamna maendeleo ambayo serikali ya gavana Lonyangapuo imeafikia licha ya kupokea kiwango kikubwa cha fedha hizo ikilinganishwa na mtangulizi wake Simon Kachapin.
Poghisio ametishia kuweka wazi kwenye vyombo vya habari kile amedai kuwa maovu ambayo yamekuwa yakifanyika katika serikali ya gavana Lonyangapuo akiwataka wakazi wa kaunti hii kuwa makini na viongozi ambao watawachagua katika uchaguzi mkuu wa mwezi agosti.