SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI YASHUTUMIWA KWA KUITELEKEZA HOSPITALI YA KAPENGURIA.


Serikali ya kaunti hii ya Pokot magharibi imeendelea kushutumiwa kwa kuitelekeza sekta ya afya hasa hospitali ya Kapenguria ambako kunatajwa kutolewa huduma duni za matibabu kufuatia ukosefu wa vifaa vya kutosha vya matibabu.
Wa hivi punde kuzungumzia swala hilo ni aliyekuwa mwakilishi wadi maalum Lucy Lotee ambaye ameelezea kusikitishwa na hali ilivyo hasa katika kitengo cha kuwahudumia wagonjwa wenye matatizo ya figo, ambapo wahudumu katika kitengo hicho wanapitia wakati mgumu kuwahudumia wagonjwa.
Lotee amedai kuwa wagonjwa wanaotafuta huduma hizo wanalazimika kununua dawa katika maduka ya kuuza dawa nje ya hospitali ya Kapenguria kabla ya kuhudumiwa.
Wakati uo huo Bi. Lotee amemtaka gavana Lonyangapuo kutimiza ahadi yake ya kuwapa bima ya afya kina mama wajane, walemavu, pamoja na wale ambao hawana ajira kwani wengi wao wanapitia wakati mgumu kutafuta huduma za matibabu kufuatia hali yao ya kiuchumi.