SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI YAPANIA KUANZA AWAMU YA PILI YA CHANJO YA MIFUGO


Serikali ya kaunti hii ya Pokot magharibi kupitia wizara ya kilimo inapania kurejelea shughuli ya kuchanja ng’ombe katika taifa la Uganda hasa maeneo ambako wafugaji kutoka jamii ya Pokot wanaishi.
Waziri wa kilimo kaunti hii ya Pokot magharibi Geofrey Lipale amesema kuwa yapo maeneo ambako maafisa walioendeleza awamu ya kwanza ya zoezi hilo hawakufika ikiwemo Amudat, Moroto na Bukwo akisema ndio maeneo ambayo yatalengwa zaidi katika awamu ya pili.
Lipale amesema kuwa walifanikiwa kuchanja jumla ya ng’ombe alfu 108,800 dhidi ya ugonjwa wa CBPP, idadi ambayo amesema kuwa iliafikiwa kutokana na ushirikiano ambao ulikuwepo kati ya maafisa kutoka kaunti hii na wale kutoka taifa jirani la uganda.
Wakati uo huo Lipale ametoa wito kwa wafugaji kuhakikisha kuwa ng’ombe wanaoaga dunia kutokana na ugonjwa wasiofahamu wanazikwa ili kuzuia kutapakaa mizoga inayoweza kupelekea kusambaa magonjwa ya mifugo na kupelekea mifugo zaidi kuaga dunia.