SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI YALENGA KUJENGA KITUO KIPYA CHA AFYA MJINI MAKUTANO
Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi inaendeleza mikakati ya kujenga kituo kipya cha afya mjini Makutano lengo kuu likiwa kupunguza msongamano katika hospitali ya Kapenguria.
Akizungumza wakati akikagua eneo ambako kituo hicho kinatarajiwa kujengwa, gavana Simon Kachapin alisema kwamba hii ni mojawapo ya hatua za kutimiza ahadi yake ya kuhakikisha kwamba huduma zinaletwa karibu na mwananchi.
“Wakati wa kampeni za mwaka jana tuliahidi wakazi wa Makutano na eneo hili kwa jumla kwamba tutajenga hospitali hapa mjini Makutano ambayo itasaidia kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali ya Kapenguria. Tumepata sehemu ambapo tutajenga hiyo hospitali ambapo shughuli hiyo itaanza hivi karibuni.” Alisema Kachapin.
Aidha Kachapin alielezea mipango ya serikali yake kutekeleza mipangilio katika mji wa Makutano ili kuhakikisha kuwa kunapatikana nafasi bora ya kuendeleza miradi muhimu kama huu kwa manufaa ya wakazi wa kaunti hiyo na vizazi vijavyo.
“Ni lazima tupangilie mji wetu ili tuwe na nafasi bora ya kutekeleza miradi muhimu kama huu ambayo itasaidia wakazi wa eneo hili pamoja na vizazi vijavyo.” Alisema.
Wakati uo huo Kachapin alipongeza huduma za kituo cha damu cha setlight ambacho alisema kwamba kimekuwa cha umuhimu mkubwa kwa wakazi wa kaunti hiyo pamoja na kaunti jirani.