Serikali ya Pokot Magharibi yakabidhiwa vifaa vya kuwasaidia walemavu

Na Benson Aswani,
Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi imepokea msaada wa vifaa vya kuwasaidia watu wanaoishi na ulemavu kutoka kwa shirika la Hope Mobility Kenya, ambavyo inatarajiwa kuvisambaza maeneo mbali mbali ya kaunti hii kuwafaa watu hao.
Akizungumza baada ya kupokezwa vifaa hivyo kwa niaba ya gavana wa kaunti hiyo Simon Kachapin, naibu gavana Robert Komole alisema takriban watu 400 watanufaika na vifaa hivyo ambavyo vinajumuisha viti 300 vya magurudumu na magongo 100 ya kutembelea (Crutches).
Aidha Komole alipongeza shirika hilo kwa msaada huo aliosema ni wa manufaa makubwa kwa kaunti hiyo ikizingatiwa haingezeweza kufikia hatua hiyo, akielezea kujitolea serikali ya gavana kachapin kushirikiana na mashirika mbali mbali kwa manufaa ya wakazi wa kaunti hiyo.
“Nachukua nafasi hii kuwashukuru hawa watu wa home mobility kwa sababu wameweza kushirikiana na serikali ya kaunti na kutupa hivyo vifaa ambavyo vinatumika na watu wetu wenye ulemavu,” alisema Komole.
Wakati uo huo Komole alitoa wito kwa wazazi wenye watoto wanaoishi na ulemavu kutowaficha na badala yake kuwatoa ili waweze kunufaika na huduma mbali mbali zinazotolewa na serikali, hasa ikizingatiwa serikali ya kaunti hiyo imeshirikiana na wahisani mbali mbali kutoa huduma kwa watu wenye ulemavu.
“Tunashirikiana na wahisani mbali mbali kuhakikisha kwamba watu wetu wenye ulemavu wanapata huduma ambazo zinastahili. Kwa hivyo wazazi wenye watoto wenye ulemavu wasiwafiche. Wawalete ili waweze kunufaika na huduma hizi,” alisema.