SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI YAIMARISJHA MIKAKATI YA KUZUIA KURIPOTIWA UGONJWA WA EBOLA.

Serikali ya kaunti hii ya Pokot magharibi kwa ushirikiano na serikali kuu imeendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa ugonjwa wa Ebola ambao umeendelea kuripotiwa katika taifa jirani la Uganda hausambai hadi humu nchini.

Haya ni kulingana na gavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi Simon Kachapin ambaye amesema kwamba serikali imeweka maafisa wa usalama katika mipaka ya kaunti hii na taifa la Uganda ili kudhibiti safari za kuingia na kuondoka katika kaunti hii na Uganda.

Aidha Kachapin amesema kwamba serikali yake na ile ya Uganda zinashirikiana katika kuhakikisha kuwa wanazuia matumizi ya njia za vichochoroni baina ya pande hizi mbili mbali na kuhakikisha maafisa wa afya wamewekwa katika mipaka ili kuwapima wanaoingia humu nchini na kuondoka.

“Serikali yetu kuu na serikali ya kaunti tunashirikiana kuhakikisha kwamba kuna doria ya kutosha mipakani hasa maeneo ambayo watu hupitia na pia katika maeneo ya vichochoro tunashirikiana na wenzetu wa Uganda kuhakikisha kuwa hakuna hali ambayo huenda ikaleta wasiwasi kaunti hii.” Alisema.

Aliongeza kwa kusema, “Tumejipanga vilivyo kwa sababu maeneo ya Amudat na maeneo yote ya mipakani tumeweka wahudumu wetu wa afya ambao watahakikisha watu wanaovuka kutoka Uganda kuingia nchini wanapimwa.”

Hata hivyo kachapin amesema kwamba licha ya serikali kuimarisha juhudi za kuhakikisha kwamba ugonjwa huo hauripotiwi humu nchini, ni jukumu pia la wananchi kuhakikisha kwamba wanachukua kila tahadhari kwa kutotangamana ovyo hasa maeneo ya mipakani.

“Kile nitawaambia watu wetu ni kwamba wakati huu ambapo kuna tahadhari ya Ebola wachukue tahadhari na kutotangamana ovyo ovyo.Pia wasiwe watu wa kutovuka mipaka kila mara bila ya kujilinda kwa sababu ni ugonjwa ambao unaambukizwa kwa urahisi sana.” Alisema.