SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI YAENDELEZA SHUGHULI YA KUCHANJA NG’OMBE KARITA

Maafisa kutoka idara ya kilimo kaunti hii ya Pokot magharibi wakiongozwa na waziri wa kilimo kaunti hii Geofrey Lipale wamekita kambi eneo la Karita nchini Uganda kuendeleza zoezi la kutoa chanjo kwa mifugo ya wakazi wa eneo hilo ambao wengi wao ni kutoka jamii ya pokot.
Akizungumza wakati wa zoezi Lipale amesema kuwa chanjo hiyo dhidi ya ugonjwa aina ya CBPP itachukua takriban siku kumi na wanalenga kuchanja zaidi ya ng’ombe alfu 100 huku akitoa wito kwa wakazi wa maeneo hayo kuleta ng’ombe wao ili wapate chanjo hiyo.
Aidha Lipale amewahakikishia wakazi wa kaunti hii kuwa zoezi hilo litaendeshwa kwa mifugo wao punde tu watakapomaliza kuchanja mifugo hao upande wa Uganda akiwataka madaktari wanaoendeleza shughuli hiyo kujikakamua ili kuimaliza kwa wakati.
Wakati uo huo mbunge wa Kacheliba Mark Lumnokol amelalamikia kukithiri hali ya ukame ambayo amesema kuwa imeathiri pakubwa afya ya mifugo kwa kukosekana lishe ya kutosha na hivyo kuathiri pakubwa uchumi wa wakazi wengi ambao wanategemea mifugo kuwa pato lao.