SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI YAENDELEZA MPANGO WA KUANGAZIA MATUMIZI YA ARDHI.
Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi kupitia wizara ya ardhi inaendelea kuangazia mpango wa jinsi ardhi nzima ya kaunti hiyo itapangiliwa katika shughuli mbali mbali, mpango ambao umekuwa ukishughulikiwa kuanzia mwaka 2014.
Waziri wa ardhi, nyumba na mipangilio ya miji kaunti hiyo Esther Chelimo alisema kwamba mpango huu ni muhimu kwa wakazi kwani utasaidia katika kupangilia jinsi ardhi itatumika kwa maswala mbali mbali ikiwemo kilimo, sehemu za kuweka miji, shule na shughuli zinginezo.
Aidha Chelimo alisema kwamba mpango huu unanuia kuhakikisha raslimali ambazo zinapatikana katika kaunti hiyo ya Pokot magharibi zinatumika kwa kazi ambayo inakusudiwa, pamoja na kuona kwamba hamna anayehisi kutengwa katika matumizi ya raslimali hizo.
“County special plan inaonyesha matumizi hasa ya ardhi nzima, ambapo itatoa mpangilio wa sehemu ambazo zitatumika kwa kilimo, miji, vituo vya kibiashara shule na mengine mengi. Lengo kuu ni kuhakikisha usawazishaji wa raslimali zilizopo kaunti hii kuhakikisha kila mmoja ananufaika.” Alisema Chelimo.
Wakati uo huo Chelimo alitumia fursa hiyo kuweka wazi kwamba serikali ya kaunti inaendeleza zoezi la kusajili ardhi, ili kubaini mipaka ya kudumu kutoka kipande kimoja cha ardhi hadi kingine hali itakayowawezesha wakazi wanaomiliki ardhi hizo kupata hati miliki za ardhi.
“Kwa sasa tunaendeleza shughuli ya usajili wa ardhi ili kubaini mipaka halisi ya vipande vya ardhi kaunti hii ambapo baadaye wamiliki wa ardhi watapata wakati bora wa kupokea hati miliki za ardhi.” Alisema.