SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI YAENDELEZA MIKAKATI YA KUIMARISHA MAZINGIRA YA WAFANYIBIASHARA.

Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi kupitia idara ya biashara, viwanda, mashirika na kawi imeratibu miradi mbali mbali ambayo inanuiwa kuwanufaisha wakazi  hasa wafanyibiashara katika juhudi za kupiga jeki shughuli zao za kila siku.

Akizungumza katika kikao na wanahabari, afisa mkuu katika idara hiyo Musa Ruto alisema kwamba wizara hiyo inalenga kuanzisha shirika la mikopo kwa jina biashara mashinani, litakalotoa mikopo kwa wafanyibiashara mbali mbali kuinua biashara zao ambapo kinachosubiriwa sasa ni idhini ya bunge.

”Tunafikiria kuanzisha mkopo kwa wafanyibiashara kwenye idara hii ya biashara, unaoitwa biashara mashinani. Tunachosubiri tu ni kuidhinishwa na bunge kwani sasa kuna mswada ambao umetengenezwa.” Alisema Ruto.

Aidha Ruto alisema kwa ushirikiano na shirika la misaada la Marekani USAID, serikali inalenga kujenga soko kubwa katika mji wa Makutano ili kuwapa nafasi na mazingira salama wafanyibiashara wanaoendeleza shughuli zao kando mwa barabara.

“Tunashirikiana na mashirika mengine kama vile USAID katika kutekeleza miradi hii. Tuna mipango ya kujenga soko kubwa mjini Makutano ambalo litasaidia kuwaondoa hawa wafanyibiashara ambao wanauzia kando ya barabara ili wawe katika sehemu salama ya kuendesha shughuli zao.” Alisema.

Wakati uo huo Ruto alidokeza kuhusu mipango ya kujengwa soko la kieneo huko Marich ambalo litakuwa la manufaa makubwa kwa wafanyibiashara wa eneo hilo ikizingatiwa litawaunganisha na wafanyibiashara kutoka kaunti jirani ya Turkana na taifa la Sudan.

“Tuna mipango pia ya kujenga Soko la kieneo, huko Marich. Hili litakuwa soko muhimu zaidi kwa wakazi wa eneo hilo kwa sababu soko hili litawaunganisha na wafanyibiashara kutoka kaunti ya Turkana na taifa la Sudan ambao watakuwa wakija kununua bidhaa hapo.” Alisema.