SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI YAENDELEZA MIKAKATI YA KUIMARISHA HADHI YA MIJI.
Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi inaendeleza mikakati kwa ushirikiano na idara mbali mbali kuhakikisha kwamba miji ya kapenguria na Chepareria inaimarika hata zaidi.
Akizungumza wakati wa uteuzi wa wanachama wa bodi ya manispaa ya mji wa chepareria naibu gavana Robert Komole alisema bodi hiyo itasaidia pakubwa kuhakikisha kwamba raslimali zinatumika vyema katika kuupangilia mji huo na kutekeleza maendeleo hitajika.
Aidha Komole alimpongeza gavana Simon Kachapin kwa kuharakisha hatua ya kuufanya mji wa Chepareria kuwa manispaa hatua aliyosema kwamba itapelekea mji huo kunufaika na mgao kutoka benki ya dunia ambao utasaidia kuimarisha hadhi yake.
“Niko tayari kusaidia gavana wetu ili kuhakikisha kwamba kwa ushirikiano na idara mbali mbali, hii miji yetu hasa ya Kapenguria na Chepareria inakua. Pia nampongeza gavana kwa kuharakisha kupandisha hadhi ya mji wa Chepareria kuwa manispaa.” Alisema Komole.
Kwa upande wake waziri wa ardhi nyumba mipango na maendeleo ya miji kaunti hiyo Esther Chelimo alisema kwamba ni hatua kubwa kwa mji wa Chepareria kupandishwa hadhi hadi kuwa manispaa akisema hii ni ishara ya maendeleo kaunti hiyo.
Chelimo aidha alisema kwamba kuteuliwa kwa bodi itakayosimamia manispaa ya chepareria kutarahisisha shughuli ya kuhakikisha maendeleo katika mji huo.
“Hii ni hatua kubwa sana kwa kaunti yetu kwa mji huu kupandishwa hadhi kutoka mji hadi manispaa. Hatua hii inaonyesha kwamba kaunti hii inaendelea kuimarika kimaendeleo.” Alisema Chelimo.