SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI YAENDELEZA MIKAKATI YA KUIMARISHA BIASHARA YA BIDHAA ZA USHANGA.
Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi inaendeleza mikakati ya kuimarisha juhudi za akina mama ambao wanashona ushanga ili kuinua biashara hiyo ambayo inategemewa zaidi na kina mama wengi katika kaunti hiyo.
Waziri wa michezo, utalii, maswala ya vijana na huduma kwa jamii kaunti hiyo Joshua Siwanyang alisema kwamba serikali inaendeleza mafunzo kwa kina mama hao ambapo wamechukua watatu kutoka kila wadi katika mafunzo hayo ambao pia wataenda kuwafunza kina mama wengine katika maeneo yao kuimarisha zaidi ujuzi wao.
“Kina mama wanaoendelea kufanya kazi ya ushanga wanafanya kazi nzuri sana. Hawa wenye wako hapa wakimaliza wataenda kuwafunza kina mama wengine wajue kushona kwa sababu tumechukua kina mama watatu kutoka kila wadi kwenye mafunzo haya.” Alisema Siwanyang.
Aidha Siwanyang alisema serikali kwa ushirikiano na maafisa kutoka serikali kuu inatafuta soko kwa ajili ya bidhaa za ushanga ambazo zinatengenezwa na kina mama hao, ili kuhakikisha kwamba wananufaika zaidi na biashara hiyo.
“Kuna kikosi cha mauzo kutoka serikali kuu ambao watachukua vifaa ambavyo kina mama hawa wameshona, ndipo watusaidie kutafuta soko kwa bidhaa za ushanga.” Alisema.
Kina mama wanaohusika biashara hiyo walielezea kunufaika pakubwa na shughuli ya ushonaji ushanga wanayoitaja kuwa tegemeo lao la pekee kiuchumi hasa ikizingatiwa hawana sauti kwa mali ya familia kutokana na tamaduni za jamii.
“Sisi ni kina mama ambao hatuna chochote kule nyumbani ila tunategemea tu kazi ya mikono yetu. Kupitia ushanga sasa tunashughulikia mahitaji yetu wenyewe bila kutegemea waume zetu ama mtu yeyote.” Walisema kina mama.