SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI YAENDELEZA MAFUNZO KWA WALIMU WA ECDE KUHUSU MTAALA WA CBC.
Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi imeandaa warsha ya walimu wa chekechea ECDE ili kutoa mafunzo kwa walimu hao hasa kuhusu jinsi ya kuwashughulikia watoto kabla ya kujiunga na shule ya msingi, warsha ambayo iliandaliwa eneo la Konyao.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha hiyo, naibu gavana kaunti Robert Komole alisema serikali ililazimika kuandaa warsha hiyo kuwapa mafunzo walimu hao hasa kuhusu mtaala mpya wa elimu CBC ikizingatiwa hawakupokea mafunzo hayo awali wakati yakitolewa kwa walimu wengine.
“Tumekongamana ili kuhakikisha kwamba walimu wetu wana ufahamu kuhusu mtaala wa CBC kwa sababu mafunzo ya walimu wa ECDE hayakuwa. Walikuwa wakifanya tu mafunzo ya walimu wengine. Kwa hivyo tumeamua kama kaunti ya Pokot magharibi tuwape walimu hawa mafunzo ili waweze kufahamu vyema mtaala huu na kuwahudumia vyema watoto.” Alisema Komole.
Komole alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa serikali kuu pamoja na tume ya kutathmini mishahara ya wafanyikazi wa umma SRC kutoa maelezo kamili kuhusu mishahara ya walimu hao akisema serikali za kaunti zimeshindwa kuchukua hatua baada ya SRC kutoa taarifa za kukanganya kuhusu mishahara hiyo.
“Serikali ya kitaifa kwa ushirikiano na tume ya mishahara SRC wanafaa kuweka wazi kuhusu hatima ya mishahara ya walimu hawa, kwa sababu imekuwa vigumu kwa serikali za kaunti kuchukua hatua yoyote kutokana na taarifa za kukanganya kuhusu mishahara zilizotolewa na SRC, moja ikiagiza kuongezwa na nyingine ikiagiza kupunguza.” Alisema.
Dinah Kamatai mmoja wa walimu hao wa ECDE alisema wamekuwa wakipitia wakati mgumu kuwahudumia wanafunzi hao hasa baada ya kubadilishwa mtaala ila sasa mafunzo hayo yatawafaa zaidi.
“Tumekuwa na changamoto kuwashughulikia watoto hawa tangu kuanza kutekelezwa mtaala mpya wa elimu CBC kwa sababu sisi tulikuwa tukitumia mfumo wa awali. Ila sasa tunavyopata mafunzo haya tutakuwa katika nafasi bora ya kutekeleza majukumu yetu inavyopasa.” Alisema Kamatai.