SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI YAENDELEZA HARAKATI ZA KUWAHAMI WALIMU WA ECDE KUHUSU MTAALA WA CBC.
Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi kupitia idara ya elimu ya chekechea, early childhood development kwa ushirikiano na shirika la daughters of charity inaendeleza mafunzo kwa walimu wa chekechea kuhusu mtaala mpya wa elimu CBC.
Akizungumza na wanahabari afisa mkuu katika idara hiyo kaunti Loketuman Julius alisema kwamba mafunzo hayo yaliyoanza tarehe 14 mwezi juni katika wadi ya Endough ambayo ni moja ya maeneo ambayo yanalengwa kaunti ya Pokot magharibi, yamewanufaisha walimu 103 eneo hilo pekee.
“Mafunzo haya yalianza eneo hili la Endough tarehe 14 na tunalenga kuwafunza walimu wa chekechea kuhusu mtaala mpya wa elimu wa CBC. Tuna jumla ya walimu 103 wa ECDE ambao wamehudhuria mafunzo haya na nina imani kwamba wamenufaika.” Alisema Loketuman.
Ni kauli ambayo ilisisitizwa na mkurugenzi wa elimu ya chekechea kaunti hiyo Joseph Tonyirwa ambaye alisema mpango huo ulizinduliwa rasmi mwezi aprili mwaka huu lengo kuu likiwa kuhakikisha kwamba walimu hao wanapata ufahamu zaidi kuhusiana na mtaala wa CBC.
“Hawa walimu wameelezwa mambo mengi ambayo wanafaa kuzingatia wakati wanapoendeleza huduma zao kwa wanafunzi wa chekechea pale darasani. Tulizindua rasmi mafunzo haya mwezi aprili na yalianzia eneo la Konyao.” Alisema Tonyirwa.
Baadhi ya walimu ambao wamehudhuria mafunzo hayo walielezea kuridhishwa na huduma ambazo wamepokea wakisema kwamba ujuzi waliopokea utawafaa zaidi katika shughuli zao za kila siku kuwahudumia watoto wa shule ya chekechea.
“Tumepata ujuzi ambao utatusaidia kuwashughulikia vyema watoto wetu. Tunashukuru sana serikali ya kaunti na shirika la daughters of Charity kwa kuchukua hatua hii muhimu sana kwa walimu wa ECDE.” Walisema.