SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI YAENDELEZA HARAKATI ZA KUIMARISHA UFUGAJI.
Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi imejitolea kuhakikisha kwamba inapiga jeki shughuli za wafugaji na kuwawezesha kuimarisha hali yao ya uchumi hasa ikizingatiwa idadi kubwa ya wakazi wa kaunti hiyo wanategemea ufugaji kuwa chanzo cha mapato.
Afisa mkuu katika wizara ya kilimo, mifugo uvuvi na unyunyiziaji maji mashamba Naomi Cherotich alisema kwamba hatua ya serikali ya kaunti kuimarisha aina ya mifugo hasa ng’ombe inanuia kuhakikisha kwamba wakulima wanapata mifugo ambao watatosheleza mahitaji ya kiwanda cha nyama kinachotarajiwa kufunguliwa kaunti hiyo.
Aidha Cherotich alisema serikali ya kaunti itapeana mitungi ya kuhifadhi maziwa kwa wakulima ili kuhakikisha usalama wa maziwa yao wanaposafirisha.
“Kama kaunti tumeamua kuimarisha harakati za wakulima ili kuongeza uzalishaji hasa ikizingatiwa kwamba tuna kiwanda cha nyama ambacho tunaenda kufungua kaunti hii. Pia tunatoa mitungi kwa wakulima wa ng’ombe wa maziwa ili kuwahakikishia usalama wa maziwa yao wanaposafirisha.” Alisema Cherotich.
Wakati uo huo Cherotich alisema serikali ya kaunti kupitia wizara ya kilimo imeendelea kuweka mikakati ambayo itaboresha ushirikiano na wawekezaji ambao pia watainufaisha kaunti hiyo pakubwa kupitia shughuli zao.
“Kwa sasa tumebuni mpango ambapo wawekezaji wanatuelezea yale ambayo wanataka kufanya katika kaunti hii, ili kama idara pia tuwauzie kile ambacho tungependa kufanya ndipo watusaidie kama kaunti kwa manufaa ya watu wetu.” Alisema.