SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI YAAZIMIA KUPANDA MICHE ZAIDI MSIMU HUU


Serikali ya kauti hii ya Pokot magharibi itaendelea kupanda miche hasa katika maeneo ya milima ili kuhakikisha chemchemi za maji zinahifadhiwa, kando na kuhakikisha viwango vya misitu vinaafikiwa kaunti hii ulimwengu ukiadhimisa siku ya ardhi duniani world earth day.
Akizungumza baada ya kupokea ufadhili wa miche zaidi ya alfu 50 kutoka benki ya Equity, gavana John Lonyangapuo amesema kuwa watatumia taasisi mbali mbali ikiwemo za elimu na makanisa katika shughuli nzima ya kupanda miche na kuwa zoezi hilo litaendeshwa katika kila wadi.
Meneja wa benki ya Equity tawi la Pokot magharibi James Biwott amesema kuwa benki hiyo inalenga kupanda miche alfu 46 msimu wa mvua utakapoanza huku akitoa wito kwa wakazi wa kaunti hii kukumbatia zoezi hilo.
Kwa upande wake msimamizi wa misitu kaunti hii Allan Ongere ameipongeza benki ya Equity kwa kutoa miche kwa serikali ya kaunti akiongeza kuwa wanalenga kupanda miche milioni 3.5 kabla ya kukamilika mwaka huu 2021.
Naye waziri wa maji na mazingira Luka Chepelion amewahakikishia wakulima na makundi mbali mbali ambao waliuzia serikali ya kaunti miche mwaka jana kuwa fedha zao zitashughulikiwa juma hili.