SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI YAAHIDI KUIMARISHA MIUNDO MSINGI KATIKA SHULE ZOTE ZA MSINGI NA UPILI.
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin amesema kwamba serikali yake imetenga shilingi milioni 20 zitakazotumika kwa ajili ya ujenzi wa miundo msingi kwenye shule za msingi na upili.
Akizungumza baada ya kuikabidhi shule ya upili ya mseto ya Lityei shilingi alfu 700 kushughulikia changamoto mbali mbali ambazo zinakabili shule hiyo, Kachapin aidha alisema kwamba serikali yake itashirikiana kwa ukamilifu na serikali kuu kuhakikisha kwamba miundo msingi ya shule inaimarishwa kaunti hii.
“Mimi kama gavana nimetenga milioni 20 zitakazotumika kuimarisha miundo msingi kwa shule zetu za msingi na za upili. Mimi naahidi kufanya kazi kwa ushirikiano na serikali kuu ili kuona kwamba shule zetu zimeendelea vizuri.” Alisema Kachapin.
Aidha Kachapin alikiri kuwepo changamoto katika utekelezwaji wa mtaala mpya wa elimu CBC akielezea umuhimu wa serikali kuu kushirikiana na serikali za kaunti katika kutatua changamoto hizo na kuhakikisha utekelezwaji wa mtaala huo unafanikishwa.
“Najua kwamba mtaala wa CBC una changamoto, na serikali kuu ikishirikiana na zile za kaunti tutaweza kukabiliana kwa pamoja na changamoto hizi kuhakikisha kwamba mtaala huu unaafikia malengo hitajika.” Alisema.
Kwa upande wake mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Lityei Rose Kitui alimshukuu gavana kwa kuikabidhi shule hiyo fedha hizo ambazo alisema zitatumika katika ujenzi wa vyoo na maabara ambazo zimekuwa changamoto kubwa.
“Tumekuwa na changamoto nyingi sana katika shule hii na namshukuru gavana kwa kutuletea fedha hizi ili tuweze kuona sehemu ambayo tutashughulikia kwanza. Kwa sasa tunakosa vyoo, hatuna maabara ya kuridhisha na pia ukiona majengo mengi ni ya mabati.” Alisema Kitui.