SERIKALI YA POKOT MAGHARIBI NA UGANDA ZAWEKA MIKAKATI YA KUHAKIKISHA ELIMU KWA MTOTO WA KIKE.


Serikali ya kaunti hii ya Pokot magharibi na taifa jirani la Uganda zimeweka mikakati ya kuhakikisha kuwa visa vya ukeketaji na ndoa za mapema kwa mtoto wa kike vinakabiliwa na kumpa fursa mtoto wa kike kusoma na kuafikia ndoto zake maishani.
Mwakilishi wa jamii ya Pokot katika bunge la Uganda Mika Lolema Kasile, amesema kuwa idara za usalama upande wa Uganda ziko macho kuhakikisha kuwa mwanafunzi yeyote wa kike kutoka kaunti hii, atakayetoroshwa eneo hilo kwa lengo la kukeketwa au kuozwa anakamatwa na kurejeshwa shuleni.
Aidha Lolema ameelezea haja ya kushauriwa mapema wanafunzi kuhusu kozi ambazo wanapasa kufanya ili wawe katika nafasi nzuri ya kuchagua kozi zitakazowanufaisha maishani, wakati wanapokamilisha masomo yao ya shule za upili.
Ni kauli ambayo imetiliwa mkazo na meneja wa CDF eneo bunge la Kacheliba Wilson Koringura ambaye amesema serikali hizi mbili zimeweka mikakati ya ushirikiano, kwa lengo la kuhakikisha watoto wanaepushwa na tamaduni zilizopitwa na wakati na kuegemea zaidi masomo.