SERIKALI YA LONYANGAPUO YASUTWA KWA KUWATELEKEZA WAATHIRIWA WA MAPOROMOKO YA ARDHI.
Gavana wa kaunti hii ya Pokot magharibi Simon Kachapin ameendelea kushutumu uongozi uliotangulia kwa kuwatelekeza wakazi walioathiriwa na maporomoko ya ardhi miaka mitatu iliyopita baada ya kupatikana katika afisi za kaunti vifaa vilivyokusudiwa kupewa waathiriwa hao.
Akizungumza na wanahabari Kachapin amesema kwamba inasikitisha kuona kwamba wapo watu waliojinyima kuhakikisha kwamba waathiriwa wanasaidika ila misaada yao inakosa kutekeleza malengo yaliyokusudiwa kutokana na kutowajibika kwa waliokabidhiwa vifaa hivyo.
Kachapin amesema kwamba atashirikiana na viongozi mbali mbali ikiwemo waakilishi wadi wa maeneo ambako kulishuhudiwa maporomoko ya ardhi ili kuwatambua waathiriwa iwapo wangalipo na kuwasilisha misaada hiyo kwao.
Kachapin ametumia fursa hiyo kuelezea mikakati ambayo serikali yake inaweka kuhakikisha kwamba hakushuhudiwi tena majanga kama hayo kaunti hii ya Pokot magharibi, ikiwemo kuwahusisha wadau kuwahamasisha wakazi kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira.