SERIKALI YA KAUNTI YA POKOT MAGHARIBIWA YASUTWA KWA KUDORORA SEKTA YA AFYA
Siku chache tu baada ya maafisa kutoka wizara ya afya kaunti hii ya Pokot magharibi kufika mbele ya bunge la kaunti hii kuhusu afya kujitetea kufuatia madai ya kutelekezwa idara ya afya hasa hospitali ya Kapenguria, seneta wa kaunti hii Samwel poghisio ameendelea kuibua maswali kuhusu hali ya hospitali hiyo.
Akizungumza na kituo hiki, Poghisio amesema hospitali hiyo iko katika hali ya kusikitisha hali ambayo inapelekea wagonjwa wengi wanaotafuta huduma za matibabu kulazimika kutafuta huduma hizo nje ya kaunti hii ya pokot magharibi.
Poghisio amekosoa hatua ya uongozi wa kaunti kwa kubadili mawaziri katika idara hiyo hali anayosema haitasaidia kwa vyovyote kutatua matatizo yanayokumba sekta ya afya kaunti hii, akimtaka gavana John Lonyangapuo kuangazia masaibu ya madaktari na wahudumu wa afya katika hospitali ya kapenguria.
Wakati uo huo Poghisio ametaka serikali ya kaunti kuwajibishwa kwa ,kile ambacho ametaja kuwa kutumia vibaya fedha zilizotengwa kwa ajili ya kutumika katika kukabilia janga la corona akisema kaunti hii haijapiga hatua zozote katika kukabili janga hilo.