SERIKALI YA KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI YAZINDUA USAMBAZAJI WA DAWA YA KIMA CHA SHILINGI MILIONI 40.

Serikali ya kaunti hii ya Pokot magharibi imezindua rasmi shughuli ya usambazaji wa dawa za kima cha shilingi milioni 40 katika zahanati mbali mbali za kaunti, ambazo ilipokea kutoka kwa shirika la kusambaza dawa na vifaa vya matibabu KEMSA.

Akizungumza wakati wa shughuli hiyo naibu gavana Robert Komole amesema kwamba dawa hizo zitasambazwa kwa zahanati 141 maeneo mbali mbali ya kaunti hii ili kuimarisha huduma za matibabu kwa wananchi.

Aidha Komole amesema kwamba watahakikisha dawa hizo zinawafikia wanaolengwa akitoa wito kwa maafisa wa afya maeneo ya mashinani kuchangia juhudi za kuhakikisha hilo.

Wakati uo huo Komole amesema serikali ya kaunti imepokea mitambo 300 ya oksijeni kutoka kwa shirika la kushughulikia maswala ya watoto Amref ambayo inatarajwa kusambazwa katika hospitali za kaunti ndogo zote ili kuwapunguzia wagonjwa gharama ya kusafiri hadi kapenguria kutafuta huduma hizo.