SERIKALI YA KAUNTI KUGHARAMIA MATIBABU YA WATOTO WALIOJERUHIWA TURKWEL KUFUATIA SHAMBULIZI LA WEZI WA MIFUGO.

Waziri wa afya kaunti ya Pokot magharibi cleah Parlklea amewahakikishia wazazi wa watoto waliojeruhiwa katika shambulizi lililotekelezwa na wahalifu eneo la Turkwel siku ya jumamosi kwamba serikali ya kaunti kupitia wizara ya afya itahakikisha watoto hao wanashughulikiwa ipasavyo.

Akizungumza wakati alipowazuru watoto hao ambao wamelazwa katika hospitali ya kapenguria, Parklea alisema wizara yake italazimika kuchukua jukumu la kuhakikisha kwamba watoto hao wanahudumiwa vyema kufuatia hali duni ya kifedha ya familia zao.

Alisema japo watoto hao walipata majeraha mabaya katika shambulizi hilo lililotekelezwa na wezi wa mifugo, hali yao imeendelea kuimarika hadi kufikia sasa mmoja wao akilazimika kusafirishwa hadi hospitali ya moi mjini Eldoret kufuatia kiwango cha majeraha aliyopata.

“Tumezuru hospitali hii kuangalia hali ya watoto wawili walioshambuliwa kwa risasi huko Turkwel. Mmoja wao alipigwa risasi shingoni na hali yake ilikuwa tete sana ikabidi tumpeleke Eldoret. Yule aliyesalia hapa hali yake si mbaya sana. Wizara ya afya itawashughulikia watoto hawa kwa sababu familia zao hazina uwezo wa kifedha kugharamia matibabu.” Alisema Parklea.

Kwa upande wake daktari mkuu wa hospitali hiyo Simon Kapchanga alihakikisha huduma bora kwa watoto hao akipongeza serikali ya gavana Simon Kachapin kwa kuhakikisha kwamba hospitali hiyo inapata vifaa vya kutosha kufanikisha shughuli za matibabu kwa wagonjwa.

“Tunamshukuru sana gavana kwa kuwekeza zaidi kwenye hospitali hii kwa sababu tangu achukue mamlaka hali imebadilika kabisa katika hospitali hii. Dawa tunazo za kutosha pamoja na vifaa ambavyo vimerahisisha huduma zetu kwa wagonjwa.” Alisema Kapchanga.