SERIKALI YA BARINGO YATAKIWA KUSAMBAZA CHAKULA KWA WAKAZI.


Wakazi katika eneo bunge la Baringo kaskazini sasa wanaitaka serikali ya kaunti ya Baringo kwa ushirikiano na ile ya kitaifa kuanzisha mpango wa kuwasambazia chakula cha msaada kwani wengi wanakabiliwa na njaa.
Wakiongozwa na Joshua Changwony kutoka Sibilo, wakazi hao wamesema kuwa wameathirika zaidi na kiangazi ambacho kinaendelea kushuhudiwa na kimechangiwa na hali ya kupotea kwa mvua katika kipindi cha miezi kadhaa sasa.
Changwony anasema kuwa wenyeji wengi wanasafiri mwendo mrefu kutafuta malisho ya mifugo na pia maji ya matumizi ya nyumbani kwani vyanzo vya maji walivyovitegemea vimekauka.
Kwa upande wake Jonathan Tokei amesema kuwa shughuli za masomo zitatatizika pakubwa iwapo serikali ya kaunti na ile ya kitaifa hazitaingilia kati na kuwasambazia wakazi chakula huku akiongeza kwamba tayari baadhi ya wanafunzi wameanza kususia kwenda shuleni kutokana na ukosefu wa chakula na maji manyumbani mwao.
Awali gavana Stanley Kiptis aliagiza idara ya kukabiliana na majanga katika kaunti hii kuanza mpango wa usambazaji wa maji kwa maeneo yaliyoathirika zaidi huku pia akiihimiza serikali ya kitaifa kuweka mikakati ya kuwasaidia wenyeji wasiokua na chakula.