SERIKALI YA BARINGO YAENDELEZA UTATHMINI WA ATHARI ZA UVAMIZI WA WEZI WA MIFUGO.


Maafisa wa idara ya dharura katika kaunti ya Baringo, wenzao kutoka shirika la msalaba mwekundi pamoja na wale kutoka mamlaka ya kitaifa ya kukabiliana na majanga NDMA wanazuru wadi ya Bartabwa ili kutathmini athari za uvamizi ambao umekuwa ukishuhudiwa kwenye baadhi ya maeneo.
Kwenye kikao na wanahabari naibu gavana kaunti ya Baringo Jacob Chepkwony amesema kuwa maafisa hao watakuwa na jukumu la kubaini idadi ya watu walioyakimbia makazi yao kutokana na uvamizi pamoja na shule zilizofungwa kufikia sasa kabla ya kuanza mpango wa kusambaza chakula cha msaada kwa waathiriwa.
Aidha chepkwony amelaani visa vya uvamizi na wizi wa mifugo ambavyo vimekuwa vikishuhudiwa katika eneo bunge la Baringo kaskazini na kusini huku akisema kwamba vimechangiwa na kiangazi ambacho kimesababisha mzozo kuhusu malisho.
Wakati uo huo chepkwony amewahimiza wahisani kujitokeza na kutoa misaada mbali mbali ya kiutu ikiwamo vyakula na mavazi itakayosambazwa kwa wakazi ambao wameathirika kutokana na utovu wa usalama.