SERIKALI POKOT MAGHARIBI YATETEA HATUA YA KUWAAJIRI WATAALAM WA KUTOA MAFUNZO KWA WAKULIMA.

Waziri wa kilimo, mifugo, uvuvi na unyunyiziaji maji mashamba kaunti ya Pokot magharibi Wilfred Longronyang amepuuzilia mbali madai kwamba kulikuwa na mapendeleo katika kuwaajiri wataalam wa kutoa ushauri kwa wakulima jinsi ya kuendeleza shughuli zao katika wadi mbali mbali.

Akizungumza na wanahabari Longronyang alisema mahojiano ya kuwatafuta wataalam hawa yalikuwa wazi, na kwamba ni afisa mmoja pekee kutoka katika wizara ya kilimo aliyehusika kwenye mchakato huo, huku wanachama 9 wa  jopo lililoendesha mahojiano hayo wakitoka miongoni mwa jamii.

Alisema kwamba serikali ya kaunti kupitia idara ya kilimo na mifugo ina nia njema kwa ajili ya wakazi, na lengo kuu ni kuhakikisha kwamba wakulima wanatekeleza shughuli zao za kilimo bila kuathirika pakubwa na mabadiliko ya tabia nchii.

“Hakukuwa na maelewano yoyote kuhusu ni nani ambaye tutaajiri na ni nani ambaye hatufai kuajiri. Watu wote waliopewa nafasi hizo walipitia mahojiano ambayo yalikuwa ya wazi na ambayo hayakuwa na mkono wa serikali. Kulikuwa na afisa mmoja pekee wa serikali katika kamati ya watu 10 walioendesha mahojiano hayo.” Alisema Longronyang.

Alitoa wito kwa viongozi hasa waakilishi wadi kushirikiana na idara ya kilimo katika kuhakikisha wakulima wananufaika na huduma za serikali, kwani lengo ni kuhakikisha kwamba wananufaika na shughuli zao za kilimo, akisema idara yake ipo tayari kurekebisha patakapotokea dosari.

“Natoa wito kwa viongozi hasa waakilishi wadi kushirikiana na serikali ili tuhakikishe kwamba wakulima katika kaunti hii wanapata matunda ya jasho lao. Lengo la serikali ni kuhakikisha kwamba kilimo kinakuwa na faida kwa watu wetu.” Alisema.