SERIKALI POKOT MAGHARIBI YAENDELEZA MIKAKATI YA KUHAKIKISHA USALAMA WA WANANCHI MVUA YA ELNINO INAPOTARAJIWA.

Serikali ya kaunti ya Pokot magharibi imeendelea kuweka mikakati ya kuzuia athari zozote ambazo huenda zikashuhudiwa wakati wa mvua ya elnino ambayo inatarajiwa kushuhudiwa maeneo mbali mbali ya nchi kuanzia mwezi Octoba kulingana na utabiri wa hali ya anga.

Katika taarifa kwa vyombo vya habari gavana Simon Kachapin alisema kwamba serikali yake imebuni kamati ya wadau kutoka sekta mbali mbali kaunti hiyo ambayo itashirikiana na idara zingine kutoka serikali kuu kushughulikia hali zozote za dharura wakati wa mvua hiyo.

“Kama serikali tumebuni kamati ya wadau kutoka sekta mbali mbali ambayo itashughulikia hali zozote za dharura ambazo huenda zikatokea wakati wa mavua ya elnino ambayo inatarajiwa kuanza mwezi octoba. Tunashirikiana pia na wadau mbali mbali kutoka serikali kuu ikiwemo shirika la msalaba mwekundu na mamlaka ya NDMA katika maandalizi haya.” Alisema Kachapin.

Aidha Kachapin alisema kwamba watafanya kazi na vyombo vya habari ambapo maafisa kutoka serikali ya kaunti watakuwa wakiwahamasisha wananchi wakati kukishuhudiwa mvua ili kusalia salama, akiwataka wakazi walio katika maeneo ambayo hushuhudiwa maporomoko ya ardhi msimu wa mvua kuhamia sehemu salama.

“Tutakuwa na maafisa kutoka serikali ya kaunti ambao watakuwa wakitumia vyombo vya habari vilivyo katika kaunti hii kuwahamasisha wananchi kuhusiana na msimu huu ili kuhakikisha kwamba watu wetu wanasalia salama.” Alisema.

Kando na kuangazia athari ambazo huenda zikatokea wakati wa mvua ya elnino, gavana Kachapin alisema serikali yake pia inaendeleza mikakati ambayo itahakikisha wakazi wa kaunti hii wanatumia msimu huo kupanda mimea itakayotumika kama lishe kwa wakazi pamoja na mifugo ili kuhakikisha usalama wa chakula.

“Tunaitazama mvua hii kutoka pande zote mbili. Wakati tunapojiandaa kukabili dharura zozote ambazo huenda zikashuhudiwa,  pia tunajiandaa kuitumia kwa manufaa yetu kupitia upanzi wa mimea, lishe ya mifugo na maswala mengine ambayo yatahakikisha usalama wa chakula kaunti hii.” Alisema.

[wp_radio_player]