Serikali itafakari upya pendekezo la kuondoa basari mikononi mwa magavana; waziri Kide

Rebecca Kide Lotuliatum Waziri wa elimu kaunti ya Pokot magharibi,Picha/Benson Aswani

Na Emmanuel Oyasi,
Waziri wa elimu kaunti ya Pokot magharibi Rebecca Kide Lotuliatum amesema idara ya elimu katika kaunti hiyo imeimarika tangu serikali ya gavana Simon Kachapin kuingia madarakani.


Akizungumza jumatatu katika shule ya upili ya subukwo katika hafla ya kusherehekea matokeo bora katika mtihani wa kitaifa kwa wanafunzi wa kidato cha nne KCSE mwaka 2024, waziri Kide alisema hali hii imechangiwa pakubwa na fedha za basari ambazo zinatolewa na serikali ya kaunti.


“Tangu serikali ya gavana Simon Kachapin kuingia mamlakani mwaka 2022, elimu yetu imeimarika sana. Hii imetokana na hatua ya gavana kuongeza fedha za basari ambazo anatoa kwa wanafunzi kaunti hii ambazo zimewasaidia sana kutumia muda wao mwingi shuleni,” alisema Bi. Kide.


Bi. Kide alisema fedha hizo zimekuwa za manufaa makubwa kwa wanafunzi wengi katika kaunti hiyo ambayo ilisalia nyuma kwa miaka mingi.


Alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa serikali kutafakari tena uamuzi wa kuondolewa basari mikononi mwa magavana.


“Tunaomba rais wetu William Ruto kutafakari tena kuhusiana na pendekezo kwamba magavana hawafai kutoa fedha za basari. Fedha hizi zimewasaidia pakubwa wanafunzi hasa katika kaunti hii ambayo ilisalia nyuma kwa miaka mingi,” alisema.


Kauli yake ilisisitizwa na mwalimu mkuu wa shule hiyo Samwel Lokware ambaye alisema matokeo bora ya shule hiyo yalitokana na hali kwamba wanafunzi walipata wakati mwema shuleni hasa baada ya kulipiwa karo kupitia basari, ikizingatiwa wengi wao wanatoka katika familia masikini.


“Familia nyingi eneo hili zinategemea mifugo kwa sababu hali ya anga hairuhusu upanzi wa mimea. Kutokana na hili wengi wa wanafunzi wamekuwa akitegemea fedha za basari ambazo zinatolewa na kaunti, na zilisaidia sana kuhakikisha wanafunzi wetu wanasalia darasani,” alisema Bw. Lokware.