SERIKALI ILIYOTANGULIA POKOT MAGHARIBI YASUTWA KWA ‘KUPORA’ MSAADA WA WAATHIRIWA WA MAPOROMOKO YA ARDHI.


Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin ameisuta vikali serikali iliyotangulia ya aliyekuwa gavana John Lonyangapuo kuhusiana na jinsi ilivyoshughulikia waathiriwa wa maporomoko ya ardhi yaliyoshuhudiwa mwaka 2019.
Akizungumza na wanahabari katika makao rasmi ya gavana, Kachapin alidai licha ya wakazi wengi kuathiriwa pakubwa na maporomoko hayo serikali ya Lonyangapuo haikuchukulia kwa uzito swala hilo kwani misaada mingi iliyotolewa na wahisani ingali afisini huku bidhaa zingine zikiporwa.
“Nilishangaa kuona kwamba baadhi ya misaada iliyoletwa na wahisani haikupeanwa kwa walioathirika na maporomoko ya ardhi yaliyoshuhudiwa mwaka 2019. Nimepata ripoti kwamba hata baadhi ya misaada iliporwa na tumepata hapa vichache tu. Hii sielewi ni roho ya aina gani mtu anaweza kuwa nayo.” Alisema Kachapin.
Kachapin alisema kwamba serikali yake imefanya uchunguzi na kuwatambua walengwa na sasa inanuia kuanza harakati za kuhakikisha msaada huo unawafikia, akitumia fursa hiyo kuwaahidi wahisani kwamba hali kama hiyo haitatokea katika utawala wake.
“Tumewatambua baadhi ya waathiriwa wa mkasa huo na tunawapelekea vifaa vilivyosalia kwa sababu waathiriwa bado wanahangaika hadi sasa. Na nawahakikishia wahisani wote kwamba hali hii haitarudiwa katika utawala wangu.” Alisema Kachapin.
Kwa upande wake naibu gavana Robert Komole alielezea kusikitishwa na hali hiyo akisema hatua ya gavana Kachapin kuamua kuhakikisha msaada huo unawafikia walengwa ni dhihirisho la uwazi wa serikali yake katika kushughulikia changamoto zinazowakabili wakazi.
“Namshukuru gavana kwa sababu amesema kuliko kuendelea kuficha msaada huu wacha tuwape walioathiriwa. Najua haitatosha waathiriwa wote lakini kutokana na uwazi, ameona ni heri wapate kilichokuwa chao.” Alisema Komole.