SENETI YALAUMIWA KWA MAPUUZA YA KETER NA MUNYES.


Mbunge wa Endebes kaunti ya Trans nzoia Robert Pukose amelaumu bunge la seneti kutokana na hatua ya mawaziri chales Keter wa kawi na mwenzake wa petroli na uchimbaji madini John Munyes kudinda kufika mbele ya kamati ya bunge hilo kuhojiwa kuhusu kupanda gharama ya mafuta nchini.
Pukose amesema kuwa bunge la seneti limebuni kamati ambazo zipo katika bunge la kitaifa na kutekeleza majukumu ya bunge la taifa wakati ambapo linatarajiwa kutekeleza majukumu ya uangalizi wa serikali za kaunti.
Amesema hatua hii imechangia wawili hao kupuuza miito ya kufika mbele yake kutokana na hali kuwa bunge la seneti halina sheria za kulipa uwezo wa kuwachukulia hatua mawaziri hao.
Amelitaka bunge hilo kuangazia tena sheria ambazo zinaliongoza na kubuni kamati zitakazoshughulikia maswala ya serikali za kaunti ili kuzuia hali ambapo bunge hilo linakinzana kimajukumu na bunge la kitaifa.