SENETA POGHISIO ASHTUMU VIONGOZI WA KISIASA WANAOENDELEZA SIASA CHAFU KAUNTI HII YA POKOT MAGHARIBI


Seneta wa Kaunti hii ya Pokot Magharibi Daktari Samuel Poghisio amegadhabishwa na siasa chafu zinazoendeleshwa na baadhi ya viongozi katika kaunti hii akiwataka kukoma kuendeleza siasa za chuki na kutajataja jina lake kiholela.
Ametumia fursa hiyo kumsuta vikali mbunge wa Pokot Kusini David Pkosing kwa kumbandikia madai kuingilia kati masuala ya uajiri wa machifu, madai ambayo amesema hayana msingi wowote.
Amemtaka Pkosing kutuliza siasa za kumpiga vita akimweleza kwamba siasa zake zingali changa na zitachukua muda mwingi sana ili kufika kiwango cha kumpiga vita kisiasa.
Vilevile amemtaka mbunge wa Kacheliba Mark Lomunokol kuacha wasiwasi katika uongozi wake kwani haijafika wakati wa kuyazungumzia masuala ya kisiasa ambapo amesema utakapofika wakati huo, mambo yatawekwa parwanja kuhusu ni nani anafaa kuwania wadhifa huo ujapo uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Poghisio amemsuta Lomunokol kwa madai ya utumizi mbaya wa pesa za CDF ambapo amedai kwamba hajatekeleza masuala yanayowahusu wakazi wa Kacheliba, badala yake ametumia nyingi za fedha hizo kujinufaisha binafsi.
Amemwaarifu kuwa tayari kujibu maswali kuhusu matumizi ya pesa hizo uchunguzi utakapoanzishwa siku chache zijazo.