SEFA YAZINDUA UJENZI WA BWAWA ORWO POKOT MAGHARIBI.


Shirika la SEFA limezindua ujenzi wa mradi wa unyunyiziaji maji mashamba wa parasany eneo la Orwo katika kaunti hii ya Pokot magharibi ili kuwawezesha wakulima eneo hilo kuendesha shughuli za kilimo bila tatizo la ukosefu wa mvua.
Akizungumza wakati wa kukagua ardhi ambako mradi huo unatarajiwa kutekelezwa afisa katika shirika hilo Beatrice Hadeny amesema tayari wakulima 40 watakaonufaika na mradi huo wamechaguliwa akiongeza kuwa kiwango cha kutekeleza mradi huo kitaongezwa siku za usoni kutokana na idadi ya wakulima.
Hadeny amewahimiza kina mama pia eneo hilo kujihusisha pakubwa katika kilimo ili kuwa na uhakika wa chakula cha kutosha hivyo kukabili tatizo la utapia mlo na kuhakikisha afya ya watoto wao.
Mwanakandarasi anayetekeleza shughuli hiyo William Lawrence kutoka Erico international limited ameahidi kuwahusisha wakazi wa eneo hilo katika mradi huo ambao utachukua takriban miezi sita kukamilika.