SEFA YAZINDUA MRADI WA MAEMBE YA KISASA LOMUT POKOT MAGHARIBI


Shirika la SEFA ambalo ni mshirika wa Northern Rangeland Trust NRT limezindua mradi wa upanzi wa maembe ya kisasa eneo la lomut kaunti hii ya Pokot magharibi katika juhudi za kuinua viwango vya kilimo cha zao hilo kaunti hii.
Akizungumza baada ya kutoa mafunzo kwa wakulima pamoja na kutoa miche ya mme huo, afisa katika shirika hilo Beatrice Hadeny amesema kuwa mradi huo ambao umefadhiliwa na muungano wa bara ulaya EU unalenga pia kuboresha mapato ya wakulima kutokana na zao hilo hasa ikizingatiwa uwepo wa kiwanda cha maembe eneo hilo.
Wakati uo huo Hadeny amepongeza serikali ya kaunti hii ya Pokot magharibi kupitia wizara ya kilimo na ile ya maji kwa kushirikiana na shirika hilo hali anayosema imepiga jeki pakubwa shughuli za shirika hilo kaunti hii.
Ni mradi ambao umepongezwa na afisa katika idara ya misitu eneo la Pokot kaskazini Palokapel Simon ambaye amesema utainua pakubwa hali ya maisha ya wakazi wa eneo hilo kauli ambayo imeungwa mkono na afisa katika wizara ya kilimo katika wadi ya Lomut Evangelista Lorien.