RUTO: TUTAYAPA MATAKWA YA WANANCHI KIPAU MBELE KATIKA KUTEKELEZA MIRADI YA MAENDELEO.

Waziri wa barabara katika kaunti ya Pokot magharibi Joshua Ruto amesema serikali ya kaunti hiyo itatekeleza miradi yake ya maendeleo kulingana na matakwa ya wananchi.

Akizungumza eneo la Chepareria wakati wa shughuli ya kupata maoni kutoka kwa wananchi kuhusu sehemu ambazo wangependa zipewe kipau mbele katika utekelezwaji miradi, Ruto alisema kwamba ni kupitia vikao vya kupata maoni kutoka kwa wananchi ambapo serikali ya kaunti itaweza kutimiza matakwa ya wananchi.

Aidha Ruto alisema ni hitaji la katiba kwamba wananchi wanafaa kuhusishwa kabla ya kutekeleza miradi yoyote ya maendeleo kwani ndio walio na mamlaka makuu.

“Kikatiba ni lazima tuhusishe wananchi kabla ya kutekeleza miradi yoyote ya maendeleo, kwa sababu katiba imewapa wananchi mamlaka makuu. Hao ndio wanaoidhinisha jinsi bajeti inavyoandaliwa. Kwa hivyo ni lazima tuhusishe wananchi kila mara.” Alisema Ruto.

Wakati uo huo waziri Ruto alisema maswala ya afya, barabara na maji ndio yamepewa kipau mbele na wananchi katika vikao mbali mbali ambavyo vimeandaliwa hadi kufikia sasa, na kwamba serikali itatilia mkazo sehemu hizo miongoni mwa maswala mengine.

“Kipindi chote ambacho tumekuwa tukitafuta maoni kwa wananchi kuhusu utekelezwaji wa miradi, maswala ya afya, barabara na maji ndio yanayopewa kipau mbele na wananchi kwamba hayo yakishughulikiwa itakuwa bora zaidi.” Alisema.