RUTO APONGEZA UCHAGUZI WAKE AKIMIMINIA SIFA IEBC.


Rais mteule William Samoei Ruto amewapongeza wakenya ambao walijitokeza kupiga kura na kuhakikisha kuwa anatwaa uongozi wa taifa hili.
Akizungumza baada ya kutangazwa rasmi kuwa rais wa tano wa taifa hili, Ruto alisema kuwa ushindi aliotwaa si wake bali ni wa wakenya wote waliotaka mabadiliko nchini.
Ameipongeza tume ya uchaguzi IEBC kwa mabadiliko ambayo ilifanya kwenye uchaguzi wa mwaka huu huku akimmiminia sifa mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati kwa ujasiri aliouonyesha katika usimamizi wa uchaguzi huo.
Aidha Ruto amepongeza wadau wote waliofanikisha shughuli hiyo ikiwemo viongozi wa kidini ambao amesema kuwa walihusika pakubwa katika shughuli nzima ya uchaguzi, waangalizi wa humu nchini na kimataifa pamoja na mabalozi wa mataifa mbali mbali.
Wakati uo huo Ruto amewashukuru wapinzani wake hasa Raila Odinga huku akiahidi kushirikiana na viongozi wote waliochaguliwa pamoja na watakaokuwa upande wa upinzani kuhakikisha kuwa wakenya wanapata huduma bora.