RISASI 749 ZANASWA MARICH ZIKISAFIRISHWA KUELEKEA LAMI NYEUSI POKOT MAGHARIBI.

Maafisa wa polisi katika kizuizi cha polisi cha marich kaunti ya Pokot magharibi wamenasa risasi 749 ambazo zilikuwa zinasafirishwa na mhudumu wa boda boda.

Akithibitisha kisa hicho kamanda wa polisi kaunti hiyo Peter Katam alisema kwamba risasi hizo zilikuwa zinasafirishwa kutoka eneo la Ortum kuelekea Lami nyeusi mpakani pa kaunti ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Turkana, ambako kumekuwa kukishuhudiwa utovu wa usalama.

Hata hivyo Katam alisema polisi hawakufanikiwa kumkamata mhudumu aliyekuwa akisafirisha risasi hizo baada yake kutoroka kwa kuwaona maafisa wa polisi huku akiiacha pikipiki aliyokuwa amebebea risasi hizo.

“Kuna mhudumu wa boda boda ambaye alikuwa akitokea eneo la Ortum Kueleka lami nyeusi na alipofika kwenye kizuizi cha Marich na kuwaona polisi akaacha pikipiki na kutoweka. Hao maafisa walipofika kufahamu ni kwa nini mhudumu huyo alitoroka wakapata risasi 749 ambazo alikuwa akisafirisha.” Alisema Katam.

Alisema kwamba polisi wanaendelea kumsaka mshukiwa ili awape taarifa kuhusu zilikotoka risasi hizo, wahusika wakuu na kazi ambayo zilikusudia kufanya.

“Tunamtafuta mhudumu huyo ili atupe taarifa zaidi kuhusu risasi hizi maana ni lazima kuna watu ambao walikuwa wakimtumia kuzisafirisha. Tunataka tujue kazi ambayo risasi hizi zilikusudia kufanya hasa huko lami nyeusi.” Alisema.

Itakumbukwa kwamba kumekuwepo na shinikizo kutoka kwa baadhi ya viongozi wa kisiasa kaunti hiyo ya Pokot magharibi za kuondolewa kizuizi hicho cha marich.

Eneo la Lami nyeusi na maeneo mengine ya mipakani pa kaunti hiyo na kaunti jirani ya Turkana yamekuwa yakishuhudia utovu wa usalama kwa muda sasa, huku wakazi wakilaumu viongozi wa kisiasa kwa kile wanasema kuchochea uhasama miongoni mwa wakazi.