Ripple effect yabadili desturi ya ufugaji hadi kilimo cha mimea Pokot magharibi

Mboga ya sukuma wiki katika shamba la mmoja wa wakulima, Picha/Benson Aswani
Na Benson Aswani,
Wakulima mbali mbali eneo la Kamito kaunti ya Pokot magharibi wamenufaika na mafunzo ya kilimo kutoka kwa shirika la Ripple effect Kenya kuhusu mbinu bora za kilimo katika juhudi za kuafikia lishe bora na kukabili utapia mlo miongoni mwa jamii.
Akizungumza katika hafla hiyo iliyoandaliwa kwenye boma la mkulima mmoja eneo hilo la Kamito, meneja wa miradi wa shirika hilo Alfred Juma alisema kando na kukabili utapia mlo, mafunzo haya yanalenga kuwapa uwezo wakulima kujiwezesha kifedha kupitia kilimo ili kukidhi mahitaji ya familia zao.
“Tuna mbinu na mikakati ya kufunza wakulima ili wawe na chakula cha kutosha, wawe na lishe bora, wawe na mapato ya juu ndipo waweze kuendeleza miradi yao, ili pia watoto wetu waweze kusoma,” alisema Bw. Juma.
Kulingana na waziri wa kilimo kaunti hiyo Wilfred Longronyang, lengo la mafunzo haya ni kuwawezesha wakazi kubadili mawazo ya kutegemea ufugaji kuwa kitega uchumi chao na kuzingatia kilimo cha mimea anachosema kwamba ni suluhu kwa changamoto zinazoambatana na ufugaji.
“Lengo letu hasa ni kuhakikisha kwamba wakazi kaunti hii wanatoka katika mawazo ya kutegemea ufugaji kwa kipato chao na kuzingatia kilimo, kwa sababu kupitia kilimo wataweza kushughulikia hata changamoto ambazo hushuhudiwa katika ufugaji hasa wakati wa kiangazi,” alisema Longronyang.
Baadhi ya wakulima ambao wamenufaika na mafunzo ya shirika hilo wakiongozwa na Lucy Lokile, walielezea ufanisi ambao wameafikia katika shughuli zao za kilimo tangu lilipoanza harakati zake kaunti ya Pokot magharibi.
“Tumepata maarifa ya kutekeleza kilimo kupitia wataalam hawa wa Ripple effect, na sasa tunaweza kusema kwa ujasiri kwamba tumepiga hatua nzuri katika kukabili utapia mlo, kwani sasa tunazingatia lishe bora kwa sababu tuna chakula cha kutosha,” alisema Lokile.