‘REKODI YA MAENDELEO YA WAGOMBEA NDIYO ITAKAYOAMUA HATIMA YAO’, WASEMA WAKAZI LOMUT.


Wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi wametakiwa kuwa makini na kuwapiga msasa viongozi wote wa kisiasa ambao wametangaza nia ya kugombea nyadhifa za uongozi katika uchaguzi mkuu wa mwezi agosti ili kuwachagua viongozi wenye nia ya kuimarisha maisha ya wakazi.
Wakiongozwa na Lomeri Kaperur mkazi wa eneo la Lomut, baadhi ya wakazi wamesema kuwa ni wakati viongozi wanafaa kuchaguliwa kulingana na rekodi yao ya maendeleo, akidai wapo baadhi ya wanasiasa ambao wanatumia fursa waliyopewa na wananchi kujiimarisha wenyewe kwa kupora mali ya umma.
Amesema hulka hii inapasa kukomeshwa katika uchaguzi wa tarehe 9 mwezi agosti kwa mwananchi kutekeleza jukumu lake la kidemokrasia kumchagua kiongozi mwenye nia ya kutekeleza maendeleo.
Wakati uo huo kaperur ameshutumu kile anachodai tamaa ya mamlaka kwa baadhi ya jamii katika kaunti hii ambazo zinawasimamisha watu kutoka familia moja kwa kila wadhifa wa kisiasa unaowaniwa swala analosema kuwa halitokubalika na wapiga kura.