RASLIMALI NA MIPAKA YATAJWA KUWA VYANZO VYA UTOVU WA USALAMA MIPAKANI PA POKOT MAGHARIBI NA TURKANA.

Viongozi wa kaunti ya Pokot magharibi wameitaka serikali kufanikisha maendeleo hasa maeneo ya mipakani ambako kumekuwa kukishuhudiwa utovu wa usalama kama moja ya mikakati ya kutia kikomo kwa uvamizi wa kila mara.

Wakiongozwa na mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto, mwenzake wa sigor Peter Lochakapong na David Pkosing wa Pokot kusini, viongozi hao walisema uvamizi ambao unashuhudiwa maeneo hayo unatokana na rasilimali ikizingatiwa wengi wa wakazi wa maeneo hayo ni wafugaji.

Aidha walitumia fursa hiyo kutoa wito kwa serikali kubainisha ulipo mpaka baina ya kaunti ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Turkana.

“Mara nyingi swala la maendeleo na raslimali ndio tatizo kuu linalosababisha hali ya utovu wa usalama maeneo haya. Wengi wa wakazi eneo hili ni wafugaji na sasa wanang’ang’ania raslimali. Pia serikali inapasa kutusaidia kubaini uliko mpaka wa kaunti hii ya Pokot magharibi na Turkana kwa sababu hiki ni chanzo kingine cha uvamizi.” Walisema.

Kwa upande wake kamishina wa kaunti hiyo Apolo Okelo alitoa wito kwa wananchi pamoja na viongozi kuipa muda serikali kutekeleza matakwa yao, akitoa hakikisho la kushughulikiwa matakwa yanayoshinikizwa katika juhudi za kuhakikisha amani inadumishwa.

“Nina imani kwamba tukienda mbele, haya ambayo yameibuliwa na wakazi pamoja na viongozi hapa yatatekelezwa. Ingawa yote hayawezi kutekeleza mara moja, wacha tuipe serikali muda ili itekeleze yale ambayo inaweza kwa wakati huu.” Alisema Okelo.