RAIS RUTO ALAUMIWA KUFUATIA KUPANDA GHARAMA YA MAISHA NCHINI.

Hisia mseto zimeendelea kuibuliwa miongoni mwa wananchi kuhusu mapendekezo ya kuongezwa viwango vya ushuru na matozo mbali mbali kwa wakenya kama njia moja ya kufanikisha shughuli za serikali.

Wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi wakiongozwa na david Ochieng walisema kwamba hatua hii inalenga kuwaongezea wananchi mzigo ikizingatiwa tayari mwananchi wa kawaida anapitia hali ngumu kufuatia kupanda gharama ya maisha.

Waliisuta serikali ya Kenya kwanza chini ya rais William Ruto kwa kile walidai kulazimisha matozo mbali mbali kwa mishahara ya wakenya bila ya kuwahusisha wananchi wenyewe.

“Rais anavyoendelea kuongeza ushuru anawaumiza sana wananchi wa kawaida,ikizingatiwa hali ya uchumi ya sasa ambapo wengi wa wakenya wanapitia hali ngumu kujikimu kimaisha. Matozo anayoweka kila mara anapasa kuwahusisha wakenya na kukoma kuwalazimisha kulipia.” Alisema Ochieng.

Hata hivyo baadhi ya wakazi walielezea kuunga mkono mikakati ya rais Ruto kufufua uchumi wa taifa wakisema kwamba wengi wa wanaopinga hatua anazochukua rais ni watu ambao wamekuwa wakikwepa kulipa ushuru.

“Watu wanaopinga utawala wa rais William Ruto kuhusu maswala ya kulipa ushuru,ni watu ambao hawajakuwa wakilipa ushuru. Iwapo watu watakosa kulipa ushuru serikali itafanikisha vipi huduma zake kwa wananchi? Watu walipe ushuru waache kulalamika.” Walisema.