RAIS KENYATTA ATARAJIWA KUZINDUA MIRADI MBALI MBALI TRANS NZOIA


Rais uhuru Kenyatta ameratibiwa kuzuru eneo la magharibi ya nchi na kunti ya Trans nzoia kukagua na kuzindua miradi mbali mbali ya maendeleo.
Akizungumza na wanahabari mjini Kitale mshirikishi wa utawala eneo la bonde la ufa George Natembeya amesema kuwa baadhi ya miradi hiyo ni barabara ya Kitale Endebes hadi Swam wa shilingi bilioni 4.5, barabara ya Lesos Namanjalala, Kolongolo, Chepchoina ya kima cha shilingi bilioni 2.3, na ule wa maji wa kolongolo kiptogot ambao utakapokamilika utafaidi zaidi ya familia alfu 200 kupata maji safi.
Mradi mwingine ni ule wa ukarabati wa uwanja wa ndege mjini Kitale wa shilingi milioni 221 unaoendelea sawa na ule wa ujenzi wa afisi ya forodha na soko kwenye eneo la swam katika mpaka wa Kenya na Uganda utakaogharimu takriban shilingi milioni 100.
Kuhusu swala la umiliki wa ardhi, Natembeya amesema rais Kenyatta atazindua shughuli ya kuwapa wamiliki wa mashamba hati miliki ikiwemo lile la Nyakinywa.
Aidha amesema kuwa serikali inashughulikia tatizo la umiliki wa shamba la Kitalale na shamba lenye utata la chepchoina la ekari alfu 15.