RAIS ATAKIWA KUCHUKUA HATUA NA KUMALIZA MARA MOJA ‘MCHEZO’ WA RAILA.

Mwakilishi wadi mteule kaunti ya Pokot magharibi Elijah Kasheusheu ametoa wito kwa rais William Ruto kusimama kidete na kukabiliana na vinara wa chama cha muungano wa azimio la umoja one Kenya ambao anadai kwamba wanavuruga nchi kupitia maandamano wanayoendeleza.

Kulingana na Kasheusheu kinara wa muungano huo Raila Odinga amekuwa tatizo kwa serikali zilizotangulia kwa miaka mingi na sasa ni wakati rais William Ruto anapasa kutumia mamlaka yake ya amiri jeshi mkuu wa majeshi ya Kenya na kumchukulia hatua.

Alisema kwamba ni jukumu la rais kuhakikisha kwamba usalama na mali ya wakenya imelindwa kutokana na uharibifu ambao unasababishwa na mrengo wa upinzani kupitia maandamano ya kila mara.

“Nataka kumwambia rais atumie mamlaka yake ya amiri jeshi mkuu kuhakikisha kwamba mchezo ambao umekuwa ukiendelezwa na kinara wa azimio Raila Odinga kwa miaka mingi kusumbua serikali unafika kikomo. Kwa sababu mtu mmoja hawezi kushinda akihangaisha watu kwa maandamano ya kila mara.” Alisema Kasheusheu.

Kasheusheu aliwataka viongozi wa upinzani kumheshimu rais na kumpa nafasi ya kuwashughulikia wananchi ili kutimiza ahadi alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita kwani yuko afisini kufuatia imani ya wakenya wengi waliompigia kura.

“Hawa viongozi wa azimio wanafaa kufahamu kwamba rais alichaguliwa kwa njia ya halali na wakenya tarehe 9 mwezi agosti. Wanafaa kumheshimu na kumpa nafasi ya kuwatekelezea wakenya ahadi ambazo alitoa wakati wa kampeni.” Alisema.

[wp_radio_player]