RAIS ASUTWA KWA UTENDAKAZI DUNI MWAKA MMOJA TANGU ALIPOINGIA AFISINI.

Baadhi ya wananchi katika kaunti ya Pokot magharibi wameendelelea kumsuta rais William Ruto kwa kile wamedai kwamba kuendelea kutoa ahadi tele kwa wakenya kila eneo analozuru hali hatekelezi ahadi hizo.

Wakiongozwa na Nicholas Kakuko ambaye ni mwanaharakati, wakazi walisema mwaka mmoja tangu rais Ruto kuapishwa rasmi kuingia afisini, ameendelea kutoa ahadi tele kwa wakenya kuhusu yale ambayo analenga kutekeleza bila hatua zozote za kudhihirisha ahadi zake.

Aidha Kakuko alikosoa mpango wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu ambao serikali imetaja kuwa muhimu katika kubuni nafasi za ajira kwa vijana nchini, akisema ni kejeli kwa vijana ambao wamesoma hadi vyuo vikuu.

Aliwalaumu washauri wa rais kwa kile alisema wamefeli katika majukumu yao ya kumpa rais ushauri unaofaa kuhusiana na kile ambacho wakenya wanahitaji hasa wakati huu ambapo hali ya maisha imeendelea kuwa ngumu.

“Yote ambayo rais anasema katika ziara anazofanya maeneo mbali mbali ya nchi ni kinyume kabisa na jinsi hali ilivyo. Amekuwa akitoa ahadi bila kuzitimiza. Mwaka mmoja tangu alipoingia afisini hamna kile anachoweza kuonyesha kwamba amefanya.” Alisema Kakuko.

Wakati uo huo Kakuko alipuuzilia mbali miito ya viongozi serikalini kwa wakenya kwamba wampe rais hadi miaka miwili kabla ya gharama ya maisha kuanza kuteremka, akisema rais hajaonyesha nia ya kushughulikia gharama ya maisha ila kuendeleza kampeni za uchaguzi mkuu ujao.

“Nasikia wengine wakisema kwamba tumpe rais kipindi cha miaka miwili ndipo gharama ya maisha iteremke. Natofautiana na kauli hiyo kabisa kwa sababu rais hajaonyesha nia yoyote ya kushughulikia gharama ya maisha. Kazi yake ni kuzunguka kote nchini kuendesha kampeni za uchaguzi ujao kwa kisingizio cha kuzindua miradi ya maendeleo.” Alisema.