RAIS ASUTWA KWA ‘KUWASALITI MAHASLA’
Rais William Ruto ameendelea kupokea shutuma kutoka kwa wakenya kufuatia hatua ambazo anachukua katika juhudi zake za kuimarisha uchumi wa nchi, ambao kulingana naye ulididimizwa na serikali iliyotangulia.
Wakiongozwa na Nicholas Kakuko, baadhi ya wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi walisema kwamba mikakati anayoweka rais William Ruto ni kandamizi kwa mwananchi wa kawaida, na kinyume kabisa na ahadi yake kwamba serikali yake itawaangazia zaidi watu wenye kipato cha chini.
Aidha Kakuko alimsuta rais Ruto kwa kile alisema ni mazoea ya kuchukua maamuzi yanayokwenda kinyume cha sheria, na kusisitiza katika kuyatekeleza licha ya mahakama kusitisha utekelezwaji wa maamuzi hayo.
“Rais Ruto anafanya kinyume kabisa na jinsi alivyowaahidi wananchi kwamba serikali yake itazingatia zaidi mwananchi wa hali ya chini. Sasa amepandisha kila kitu. Akienda kwa mikutano ya umma anasema gharama ya maisha imeteremka na wakenya bado wanahangaika.” Alisema.
Wakati uo huo Kakuko aliisuta vikali serikali ya rais Ruto kwa kile alidai kuwahangaisha viongozi wa kaunti hiyo kutokana na swala zima la utovu wa usalama kanda ya bonde la Kerio, akimtaka rais kubadili mbinu ya kukabili swala la uvamizi maeneo hayo ya mipakani.
“Viongozi wa kaunti hii wamekuwa wakihangaishwa na serikali kuandikisha taarifa kila mara na idara ya DCI kwa madai ya kueneza uchochezi. Sisi tunashangaa ni kwa nini iwe tu ni viongozi wa kaunti hii wanaoandamwa, na kumekuwa na viongozi wengi kaunti jirani ambao wanazungumza kiholela.” Alisema.
Na Emmanuel oyasi.