RAILA AENDELEA KUSUTWA KWA KUWASILISHA KESI YA KUPINGA USHINDI WA RUTO.
Baadhi ya viongozi wa kisiasa katika kaunti hii ya Pokot magharibi hasa wanaoegemea mrengo wa rais mteule William Ruto wameendelea kumsuta kinara wa chama cha muungano wa azimio la umoja one Kenya Raila Odinga kwa kupinga ushindi wa Ruto kama rais wa tano wa taifa hili.
Wakiongozwa na mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto, viongozi hao wamemsuta Raila kwa kile wamedai amekuwa na mazoea ya kupinga kila uchaguzi ambao unaandaliwa nchini, huku wakikariri kwamba ruto ndiye rais mteule wa taifa hili.
Wamesema hatua hiyo ya Raila inapelekea migawanyiko miongoni mwa wakenya hali ambayo huenda ikapelekea kuhujumiwa juhudi za kuhakikisha amani inadumu nchini akitolea mfano migawanyiko ambayo inashuhudiwa miongoni mwa makamishina wa tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC.
“Nataka kumwambia Raila kwamba mahalai napokanyaga sasa imekuwa tofauti. Kila wakati akishindwa anapinga matokeo akisema yameibwa. Sasa anaanza kuleta migawanyiko miongoni mwa makamishina na hiyo ni kama kuleta vita karibu na watu. Hatuwezikubali hayo sasa.” Amesema.
Moroto ameelezea imani kuwa mahakama itatekeleza majukumu yake kulingana na sheria na kutoa uamuzi utakaodumisha ushindi wa William Ruto jinsi ambavyo imekuwa tangu uchaguzi wa mwaka 2013 ikizingatiwa ni taasisi huru.
“Kuna kesi iliyowasilishwa mwaka 2013 ikatupiliwa mbali rais akaapishwa, za mwaka 2017 japo kura zilirudiwa raia aliapishwa. Hata hii tunajua Ruto ataapishwa kwa sababu tuna mawakili wa kutosha.” Amesema.”