RAILA AAHIDI KUIMARISHA HALI POKOT MAGHARIBI AKICHAGULIWA RAIS.

Na Benson Aswani
Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga amewahakikishia wakazi wa kaunti hii ya Pokot magharibi kuwa atashughulikia maswala yote ambayo yanawakumba iwapo atachaguliwa kuongoza taifa katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Akizungumza alipokutana na wataalam pamoja na viongozi wa kaunti hii katika misururu ya ziara yake ya azimio la umoja, Raila amesema kuwa matatizo ambayo yanakumba kaunti hii yametokana na uongozi ambao ulikuwepo tangu enzi za ukoloni ambapo kaunti za maeneo kame zilitengwa pakubwa.
Raila amesema kuwa ili kuafikia usawa wa kimaendeleo katika kaunti zote nchini ni lazima kaunti ambazo zimetengwa tangu enzi za kikoloni zitengewe mgao maalum ambao utainua maeneo hayo kimaendeleo swala analosema serikali yake itaangazia.
Viongozi wa kanda hii ambao wameandama na Raila katika ziara hizo wamepigia upatu sera za Raila wakiwahakikishia wakazi wa kaunti hii kuwa watakuwa salama mikononi mwa Raila wakimtaka kiongozi huyo kutoa kipau mbele kwa maswala ya wakazi wa kaunti hii.