RAIA WA ERITREA WATARAJIWA KUFIKISHWA KATIKA MAHAKAMA YA KAPENGURIA KWA KUPATIKANA NCHINI KINYUME CHA SHERIA.


Raia 41 kutoka Eritrea walionaswa jumanne eneo la Kanyarkwat eneo bunge la Kapenguria katika kaunti ya Pokot magharibi wakiwa nchini bila stakabadhi za kuhalalalisha uwepo wao nchini wanataraji wa jumatano kufikishwa katika mahakama ya kapenguria kujibu mashtaka ya kuwa nchini kinyume cha sheria.
Kulinganana OCPD wa Kapenguria Kipkemoi Kirui, raia hao waliokuwa wakielekea jijini Nairobi walinaswa baada ya magari matatu waliyokuwa wakisafiria kukwama katika mto Kaptarin ambapo wawili kati yao pamoja na mtoto wa takriban miaka miwili walisombwa na maji huku miili yao ikipatikana baadaye.
Kirui amesema magari matatu aina ya Land cruiser yaliyokuwa yakitumika na raia hao yamenaswa na polisi akiongeza kuwa huenda njia hiyo imekuwa ikitumiwa na raia kutoka mataifa ya kigeni kuingia nchini bila ya ufahamu wa maafisa wa polisi.
“jana jioni tulipata ripoti kwamba watu wasiojulikana walikuwa wakielekea Nairobi, wakafika mto unaitwa Kaptarin magari zao zilikwama. Polisi walipashwa habari wakaenda na walipata magari tatu. Walipochunguza walipata ni watu wametoka nchi ya Eritrea. Na walipoulizwa walikuwa wanaelekea wapi walisema walikuwa wanaelekea Nairobi.” Alisema Kirui.
Amesema raia hao watafikishwa mahakamani jumatano kujibu mashitaka ya kuwa nchini kinyume cha sheria akitoa wito kwa wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi kushirikiana na maafisa wa polisi kwa kutoa taarifa kuhusu uwepo wa watu wanaowashuku nchini ili kuimarisha usalama hasa kipindi hiki ambapo taifa linaelekea katika uchaguzi mkuu wa juma lijalo.
“Tutawapeleka kotini na tutafanya vile koti itaamuru. Kama watasema wanapelekwa huko ama watarudishwa mahali wametoka tutafata uamuzi wa koti.” Alisema kirui.
Siku ya jumanne miili ya watu watatu ukiwemo wa mtoto mwenye umri wa miaka miwili iliopolewa kutoka mto kaptarin baada ya gari walilokuwa wakisafiria kusombwa na maji.
Ni kisa ambacho kilithibitishwa na naibu chifu wa lokesheni ya tukoi David Sarakwang ambaye alisema kuwa mvua kubwa iliyoshuhudiwa usiku wa kuwamkia jumanne ilipelekea kufurika mto huo hali iliyopelekea kusombwa gari hilo.